Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amewasisitiza wakandarasi wanaojenga uwanja wa michezo Arusha kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati kabla ya ukaguzi wa mwisho wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa ajili ya AFCON 2027.
Mwinjuma ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo unaojengwa katika kata ya Olmoti, jijini Arusha.
“CAF wanakuja kufanya ukaguzi wa mwisho mwezi Julai 2026 na sisi tunataka mradi huu ukamilike mwezi Mei 2026, yaani miezi miwili kabla ya ukaguzi huo,” amesema Mwinjuma.
Amesema mradi huo ni wa kipaumbele kwa serikali na kwamba Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha ujasiri mkubwa katika kuhakikisha uwanja huu unakamilika kwa wakati.
“Mheshimiwa Rais anajua umuhimu wa uwanja huu kukamilika ili tusiwe nyuma kwenye ratiba ya CAF ya kuandaa mashindano ya AFCON 2027. Ndio maana ametuelekeza tufuatilie kwa karibu na kuhakikisha kila kitu kinalipwa kwa wakati,” alisisitiza.
Aidha, Mheshimiwa Mwinjuma alibainisha kuwa maendeleo ya mradi yanakwenda vizuri na kwamba wakandarasi wanafanya kazi kwa kasi ili kufikia malengo yaliyowekwa.
“Nimefurahi namna mradi huu unavyokwenda kwa wakati, na tunatarajia kuwa utakuwa mfano wa kuigwa kwa miradi mingine,” ameongeza.