Polisi Kaunti ya Murang’a nchini Kenya, sasa wanasema wamemtia mbaroni mshukiwa wa uhalifu, ambaye kwa mwezi mmoja sasa amekuwa akiwapora wenyeji usiku huku akiwa amejihami kwa shoka.
Mshukiwa huyo, amekamatwa baada ya waathiriwa kudai kuwa mshukiwa huyo hupapasa na kuwabusu watu anawaolenga kupora, ili wapitanjia wafikirie yeye na mlengwa ni marafiki ili kufanikisha lengo.
Kamanda wa Polisi wa Murang’a, Mathiu Kainga alisema mshukiwa huyo alitiwa mbaroni Ijumaa akiwa katika Mahakama ya Kenol wakati alipokuwa amefika hapo kujibu mashtaka mengine ya uhalifu, huku
Wenyeji wakimpa mtu huyo jina la majazi la ‘Wagathanwa Muhambati’ yaani, wa shoka mpapasaji.
Amesema, “tumemnasa jambazi na Jumatatu tutamfikisha Mahakamani kujibu mashtaka ya uvamizi, wizi wa kimabavu na kutishia maisha, amekuwa akivamia boma za watu na kuvunja dirisha kisha anamwaga petroli kwa nyumba na akishamwaga petroli, anakwambia umpitishie pesa na simu kwa dirisha la sivyo arushe moto ndani ya hiyo nyumba.”