Raia 51 na askari 11 wa Nigeria wameuawa katika vurugu zilizozuka nchini humo kufuatia siku kadhaa za maandamano ya amani ya kupinga ukatili wa polisi na wengine 37 wamejeruhiwa.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amewalaumu wale aliowaita ‘wahuni’ kwa machafuko hayo, huku akisisitiza kwamba vikosi vya usalama navyo vilijizuia kwa kiwango cha juu sana.
Buhari ameongeza kwamba maandamano hayo yaliyokuwa na nia njema, yametekwa na majambazi walioyaingilia kati, matamshi ambayo yanategemewa kuchochea mivutano zaidi.
Wanigeria wengi wameonyesha kukasirishwa na hotuba ya kitaifa ya Buhari aliyoitoa Alhamisi usiku, kwa kutokutaja vitendo vya ukatili vya wanajeshi vya kuwafyatulia risasi raia.
Katika hatua nyingine Buhari amekutana kwa mazungumzo na watangulizi wake, ikiwa ni pamoja na Goodluck Jonathan na Olusegun Obasanjo, kuhusu hali ya usalama inayoendelea nchini humo na kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais, rais Buhari amesikitishwa kuona maandamano ya amani ya vijana “yalivamiwa” na “majambazi” na ” kugeuka kuwa ya vurugu”.
Aidha, Buhari amewaonya waandamanji dhidi ya kuhujumu usalama wa kitaifa, sheria na utulivu.