Kocha mzawa Jamuhuri Kiwelu Julio amerejeshwa kwenye jukumu la kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes), ambayo itacheza michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya Sudan.
Shirikisho la soka nchini TFF limemtangaza Julio kuchukua jukumu hilo, kufuatia uzoefu alionao katika soka la Tanzania, huku huu ikiwa ni mara ya pili kushika nafasi ya kuwa kocha wa Ngongoro Heroes.
Kufuatia uteuzi huo, kocha Julio ameushukuru uongozi wa TFF chini ya utawala wa Rais Wallace Karia, huku akiahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na kila mdau wa soka nchini ili kufanikisha lengo la kuipa furaha Tanzania.
Julio amesema mbali na michezo hiyo miwiwli ya kirafiki, kikosi cha Ngorongoro Heroes ambacho kitachujwa na kubaki na wachezaji 25, kitaingia kambini kwa ajili ya kushiriki michuano ya ukanda wa Afrika mashariki na kati *CECAFA* itakayofanyika jijini Arusha baadae mwaka huu.