Watu wasiopungua 60 wamepoteza maisha nchini Chad, kufuatia kuzuka kwa ghasia baada ya vikosi vya usalama kufyatua risasi, dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali katika miji miwili mikubwa nchini humo.
Serikali ya Chad, ilitangaza amri ya kutotoka nje usiku wa jana (Oktoba 20, 2022), baada ya kuzuka makabiliano makali kati ya Polisi na waandamanaji wanaopinga uamuzi wa utawala wa kijeshi wa kuongeza madaraka.
Mamia ya waandamanaji, walikuwa wamejitokeza katika mji mkuu wa N’Djamena na miji mingine hapo jana kuadhimisha tarehe ambayo awali, watawala wa kijeshi walikuwa wameahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.
Hata hivyo, Kiongozi wa muda wa nchi hiyo, Mahamat Idriss Deby alitangaza kuongeza miaka miwili zaidi ya utawala wake huku Ufaransa, Umoja wa Afrika na mataifa mengine yakilaani ukandamizaji wa vikosi vya usalama, dhidi ya waandamanaji.