App namba moja kwa kusikiliza na kupakua muziki barani Afrika ya Boomplay inasherehekea siku ya Wanawake Duniani 2019 ikiwa na kampeni mpya ya “Boom Queens” ikiwa na lengo la kuendelea kukuza vipaji na kubadilisha tasnia Duniani.
Hayo yamesemwa na Meneja Mahusiano wa kampuni hiyo, Tosin Sorinola ambapo amesema kuwa majadiliano juu ya usawa wa kijinsia ni moja ya mambo ambayo ni muhimu kwao kama jukwaa lenye nia kubwa ya kukuza wanawake katika muziki akitolea mfano wanamuziki kama, Vanessa Mdee, Rihanna, Tiwa Savage, Fena Gitu na wengine wengi wenye vipaji ambao wameendelea kubadilisha tasnia ya muziki duniani.
Amesema kuwa App ya Boomplay itakuwa na muonekano wa tofauti hasa katika siku ya wanawake duniani tarehe 8 Machi, lengo likiwa ni kuonyesha na kukuza kazi za wanawake katika muziki na itapambwa na nyimbo, albamu pamoja na playlist za wanawake katika vipengele vyote kwenye ukurasa wa kwanza.
Aidha, amesema kuwa kampeni hiyo kabambe itatoa fursa ya kukuza mauzo ya kazi za wanawake ambao nyimbo zao zitakuwepo kwenye playlist ya Boom Queens, ambapo Playlist hiyo itakuwa na nyimbo za wasanii bora wa kike tu.
Hata hivyo, App ya Boomplay ambayo ina watumiaji zaidi ya milioni 42 dunia kote, hivi karibuni ilizindua App hiyo kwenye jukwaa la iOS huku ikijivunia kuwa nyimbo na video bora zaidi ya milioni 5 kutoka kwa wasanii wa Tanzania na Wakimataifa.