Serikali inatarajia kupeleka wataalam 100 wa kilimo nchini Israel ili kujifunza mbinu bora na teknolojia za kisasa za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji nchini.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba na Naibu Mkurugenzi Mkuu kutoka wizara ya mambo ya Nje wa Israel ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya MASHAV, Gil Haskel mara baada ya kikao.
Amesema kuwa nafasi hizo za masomo ya kilimo nchini Israel zitatoa fursa kwa wataalam hao kuongeza ufanisi katika Sekta ya kilimo nchini na kukifanya kilimo kuwa na tija zaidi.
Aidha, amesema kuwa, tatizo kubwa la Sekta ya Kilimo nchini ni uzalishaji mdogo usiokuwa na tija ambapo wakulima hutumia nguvu kubwa lakini matokeo yanakuwa madogo. hivyo, amesisitiza kuwa, wakulima nchini wanatakiwa kuzingatia mbinu bora za kilimo, matumizi sahihi ya pembejeo, mbolea na pia kutumia mbegu bora ili kuweza kumnufaisha mkulima.
Akizungumza na mgeni huyo kutoka Israel, Mgumba amebainisha kuwa, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kwa kiasi kikubwa Sekta ya Kilimo hivyo ni muhimu kilimo cha umwagiliaji kikaanza kutumika maeneo mbalimbali ya nchi kwa sababu ya uwepo wa vyanzo vya maji vya kutosha na sio kuendelea kutegemea kilimo cha mvua ili kupambana na hali hiyo.
“Hadi sasa eneo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 475,000 na Mkakati wa Serikali ni kufikia hekta milioni moja ifikapo mwaka 2035,”amesema Mgumba.
Hata hivyo, Mgumba ameiomba Serikali ya Israel kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza bonde la mto rufiji kwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili wakulima wengi waachane na kilimo cha kutegemea mvua kama ilivyo sasa.