Klabu ya Soka ya Simba, imetoa utaratibu wa jinsi mashabiki wake watakavyo shangilia kombe lao kesho Mei 25, 2019, baada ya kukabidhiwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Katika taarifa iliyotolewa leo Mei 24, 2019, na msemaji wa timu hiyo, Haji Manara, imesema kuwa mashabiki wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo dhidi ya Biashara kutoka mkoani Mara utakaoanza majira ya saa 9:00 mchana kwani kiingilio kimepunguzwa.
”Tumepunguza kiingilio kutoka 5000/= hadi 3000/= ili mashabiki wote waje kushuhudia timu yao ikikabidhiwa kombe la ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2018/19,” amesema Manara.
Aidha, Manara amebainisha kuwa kwa kuzingatia kuwa huu ni mwezi mtukufu na mashabiki wa Simba ambao wamefunga ndio maana wakaomba mchezo huo uanze mapema ili wawahi kurudi na kufuturu.
Hata hivyo, amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwenye barabara watakazopita ili kuweza kuishangilia timu yao kwakuwa kutakuwa na basi la wazi litakalokuwa linapita mitaani kutembeza kombe hilo.