Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema kuwa kuna ushahidi kwamba Iran ilihusika katika mashambulizi dhidi ya meli za kubebea mafuta katika mlango-bahari wa Hormuz wiki iliyopita.
Marekani imeituhumu Iran kuzishambulia meli mbili, moja ya Japan na nyingine ya Norway, na imetoa picha na video inayodai vinaonyesha boti za kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran wakiondoa bomu kutoka kwenye meli mojawapo, bomu ambalo halikuripuka.
Aidha, Umoja wa Ulaya ulisema video hiyo siyo ushahidi wa kutosha kuilaumu Iran, huku waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas akisema bado nchi yake inauchunguza ushahidi huo wa Marekani kabla ya kufikia hitimisho lolote.
Hata hivyo, Iran imekanusha tuhuma hizo dhidi yake kwamba imehusika na mashambulizi ya meli hizo za mafuta.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, Kansela Merkel amesisitiza kuwa kuna haja ya suluhisho la amani katika Ghuba ya Uajemi.