Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo amesema kuwa kwasasa wanatarajia kukifanya kituo cha Horohoro kuwa kituo cha pamoja (One Stop Board Post) ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea kwenye kituo hicho cha forodha kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro wilayani Mkinga mkoani Tanga ikiwemo kuzungumza na watumishi sambamba na kukikagua kituo hicho.

Amesema kuwa yapo mambo machache wanayokamilisha kabla ya kituo hicho kuanza kazi, hivyo kaahidi kwenda kuyashughulikia kwa haraka kwa kuwasiliana na taasisi, mamlaka nyingine ikiwemo upande mwingine wa wenzao wa nchi jirani ya Kenya kuhakikisha kituo hicho kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa.

“Lakini pia nimeambiwa changamoto ya Jenereta nimeambiwa inafanyiwa kazi na inakaribia kukamilika tutakaporudi Dar es salaam tutahakikisha vifaa hivyo vinafika na kufungwa suala la uhakika wa umeme litakuwa sio tatizo tena na suala la maji litashughulikiwa,”amesema Mbibo

Aidha, amewataka watumishi wa umma kwenye kituo hicho kuhakikisha wanashirikiana kwenye kufanya kazi na kutanguliza uzalendo kwenye shughuli zao ili kufikia malengo ambayo yamekusudiwa.

Mbibo ameongeza kuwa nchi haiwezi kuendelezwa na mtu mwingine isipokuwa watanzania wenyewe na kila Mtanzania sehemu aliyopo afanye kazi kwa kiwango cha juu ili waweze kuyafikia malengo yao.

Hata hivyo amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kwa nchi nzima kuhakikisha wanakuwa waadilifu kwa kiwango cha juu kwa sababu ndiyo silaha ya mafanikio yoyote na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

CCM Kagera yakunwa na utekelezaji wa Ilani
IGP Sirro afunguka kuhusu askari waliofariki kwa ajali Rufiji