Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema kuwa serikali inatambua juhudi za taasisi za dini hapa nchini ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na utulivu, hivyo itaendelea kushirikiana na taasisi hizo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika Kongamano la maombi ya wanawake waombolezao, jijini Dar es salaam, tarehe 25 Julai, 2019, ambapo Mhagama amefafanua kuwa waratibu wa Kongamano hilo wanapongezwa na viongozi wote serikalini.

“Napenda kuwahakikishia ushirikiano wa serikali katika kutekeleza majukumu yenu ya kiroho na ya huduma za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya Watanzania. Pale mtakapoona mchango wa serikali unahitajika msisite kuwasiliana nasi. Na iwapo mtaona kuna upungufu wowote semeni kwa viongozi wa wilaya, mkoa na wa kitaifa. Sisi ni wasikivu,” amesema Waziri Mhagama

Aidha, katika hatua nyingine, Mhagama amesema viongozi kwa pamoja ni shupavu, wanaoaminiwa na kutumainiwa na wananchi hasa wanyonge, ambapo viongozi wanachukia na kupinga rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwa vitendo.

Awali wakizungumza katika Kongamano hilo, waratibu wa Kongamano hilo, Mchungaji Deborah Malassy na Askofu Dkt. Godfrey Malassy wamesema kuwa wameamua kuendesha Kongamano hilo kwa kuwa wanatambua kuwa viongozi wa dini kama walivyo wa serikali wanao wajibu maalumu wa kulilea Taifa.

Kongamano hilo la kumi la Kihistoria lilihusisha Wanawake Waombolezao Kitaifa kutoka mikoa yote Tanzania  na Zanzibar, pamoja na viongozi wa Taasisi mbalimbali, limebebwa na maudhui ya  Mwaka wa Maachilio kwa Wanawake wote. Kongamano hilo ni sehemu ya Maombi ya kila mwisho wa mwaka wa tarehe 31 Disemba ya kuliombea Taifa hili yajulikanayo kama MKESHA MKUBWA KITAIFA DUA MAALUM, ambayo yamekuwa yakifanyika katika viwanja vya wazi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Zanzibar.

JPM awasihi wananchi, 'Msiibe vifaa katika mradi huu'
Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya utangazaji