Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, amesema kuwa pamoja na kwamba Tanzania imeshagundua gesi futi za ujazo trilioni 57.54 hadi sasa, bado inahitaji gesi zaidi itakayosaidia kuimarisha uchumi wa viwanda.
Ameyasema jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambapo amesema kuwa kazi ya utafutaji wa gesi inaendelea vizuri lakini akaisisitiza Menejimenti hiyo kuongeza kasi zaidi katika utafutaji wake pamoja na wa mafuta.
Waziri Kalemani ameitaka Menejimenti husika kutafuta mbinu mbalimbali na kuongeza ubunifu ili shirika hilo liweze kufanya biashara kiushindani, lipate mapato na baadaye lianze kutoa gawio serikalini.
Amesema kuwa, mwaka 2015 ilipitishwa sheria mpya ya mafuta ambayo ilibadili majukumu ya shirika kutoka kutegemea ruzuku ya serikali na kuwa shirika lenye kujiendesha kibiashara.
“Sasa, TPDC ikiwa ni kampuni ya serikali yenye kufanya biashara, ni lazima ifanye biashara kiushindani.”amesema Dkt. Kalemani
Aidha, amelitaka shirika hilo kupanua wigo wa usambazaji gesi majumbani hususani mkoa wa Dar es Salaam ambao una watumiaji wengi wa nishati ya mkaa, inayosababisha ukatwaji wa miti kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wa matumizi ya gesi kwenye magari, Dkt. Kalemani ameliagiza TPDC ifungue vituo zaidi vya kujazia gesi katika mikoa mbalimbali ili wateja walioko mikoani wapate huduma ya kubadili mfumo wa magari yao kutoka ule unaotumia mafuta na kuweka unaotumia gesi, ili kuwaepushia usumbufu wa kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam ambako ndiko kuna kituo pekee kwa sasa.
Maagizo mengine aliyotoa Waziri kwa Menejimenti hiyo ni kuandaa utaratibu wa kuachana na uagizaji nje ya nchi vifaa mbalimbali vya kusambazia gesi zikiwemo mita na mabomba, badala yake itumie vile vitakavyozalishwa nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. James Mataragio, amemhakikishia Waziri kuwa shirika lake litatekeleza kikamilifu maagizo yote aliyowapatia.
“Tayari tumeshaanza kujipanga katika maeneo yetu ya kazi yanayojumuisha utafiti, uzalishaji na biashara ya gesi. Nimerudi nikiwa na nguvu mpya kuwatumikia Watanzania,” amesema Dkt. Mataragio ambaye amerudishwa katika nafasi hiyo na Rais John Magufuli hivi karibuni baada ya kusimamishwa kwa muda.