Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) nchini Tanzania amewafutia mashtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio na wenzake wanne.
Wengine waliofutiwa mashtaka ni George Seni, aliyekuwa Kaimu Meneja wa Uvumbuzi, Welington Hudson aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Utawala, Kelvin Komba aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu na Edwin Riwa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mipango.
Mataragio na wenzake walikuwa wakikabiliwa na shtaka moja la matumizi mabaya ya madaraka ambapo ilidaiwa kati ya Aprili 8, 2015 na Juni 3, 2016 walitenda kosa hilo wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simoni amedai kuwa leo Jumatatu Agosti 19, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Kelvin Mhina kuwa shauri hilo limekuja kwaajili ya kusikilizwa lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameonyesha nia ya kutoendelea na kesi hiyo.
“Julai 10, 2019 Mkurugenzi wa Mashtaka DPP alionyesha nia ya kutoendelea na shauri hili hivyo naomba kuliondoa mahakamani chini ya kifungu cha 91(1) cha mwenendo wa makosa ya jinai,” ameeleza Wankyo
Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikiondolewa mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC), James Mataragio hakuwepo Mahakamani.
Aidha, machi 16, 2018 Mataragio na wenzake wanne walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa shtaka moja la matumizi mabaya ya madaraka, ambapo ilidaiwa kuwa walibadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa ununuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha Airborne Gravity Gradiometer Survey, katika ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo.
Ilidaiwa kuwa kwa kufanya hivyo, walikiuka kifungu cha 49(2) cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 huku ikidaiwa kwamba lengo lilikuwa ni kujipatia manufaa yasiyo halali ya Dola 3.2 milioni ambazo ni sawa na Sh7.2 bilioni.
Agosti 24, 2016 Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC, ilimsimamisha Mkurugenzi huyo kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikimkabili na Julai 22, 2019 Rais Magufuli aliielekeza wizara ya nishati kumrejesha ofisini katika wadhifa wake aliokuwa nao kabla ya kusimamishwa na kushtakiwa.