Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 50 wa Chama cha Mabunge cha Jumuiya ya Madola, Kanda ya Afrika (CPA) ambapo zaidi ya wageni 400 kutoka nchi mbalimbali wanachama wanatarajiwa kushiriki mkutano huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kuwa Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika Kisiwa cha Zanzibar kuanzia tarehe 31 Agosti hadi tarehe 5 Septemba mwaka huu.
Amesema kuwa ufunguzi wa mkutano huo utafanyika tarehe 2 Septemba, 2019 ambapo mgeni Rasmi atakuwa, Dkt. Mohamed Shein, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
“Wageni mbalimbali wamealikwa ikiwemo Maspika kutoka nchi wananchama, manaibu Spika, wabunge na mabalozi kutoka nchi wanachama pamoja na Maspika wengine kutoka mabara na Kanda nyingine,”amesema Ndugai
Aidha, amesema kuwa hadi sasa mataifa zaidi ya 13 yameshathibitisha kushiriki, huku mwitikio ukiwa ni mkubwa kutokana na Mkutano huo kufanyika Tanzania hususani katika Kisiwa cha Zanzibar.
“Naomba kuwashauri wafanyabiashara na Watanzania wenzangu kwa ujumla fursa hizi tunazozipata za kuaminiwa na mataifa mbalimbali, tuzichangamkie, ni fursa adhimu ambazo mataifa mengine wanazililia,”amesisitiza
Kwa upande wake Katibu wa Bunge ambaye pia ni Katibu wa CPA Kanda ya Afrika, Stephen Kagaigai amesema kuwa maandalizi yote yanaendelea vizuri na kwamba Sekretarieti ya CPA ipo tayari kuhudumia ugeni huo kwa ufanisi.
Kauli Mbiu ya Mkutano wa 50 wa CPA kwa mwaka huu ni “Bunge Mtandao kwa Ajili ya Kuwezesha Demokrasia”