Mkutano wa viongozi wa kundi la nchi saba tajiri zaidi duniani – G7 umeanza Jumamosi hii kusini magharibi mwa nchi ya Ufaransa.
Wachambuzi wanasema kuwa janga la moto unaoendelea kuwaka katika msitu wa Amazon, kutetereka kwa masoko ya hisa na tofauti kubwa zilizopo baina ya nchi hizo tajiri ni mambo yatakayopewa kipaumbele katika mazungumzo yao.
Mkutano huo umeanza huku kundi kubwa la waandamanaji tayari wamejipanga kuwapokea viongozi wa nchi hizo akiwemo Rais wa Marekani, Donald Trump na viongozi wenzake wa nchi za Magharibi wakati wakiwasili katika mji wa Biarritz.
Wakati huo huo polisi wamepelekwa kulinda doria ili kuzuia vurugu zozote zitakazotokea wakati wa mkutano huo.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, mwenyeji wa mkutano wa G7 ametoa shinikizo kwa Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro kuruhusu jumuiya ya kimataifa kushiriki kusaidia kuzima moto unaoendelea kuangamiza msitu wa Amazon.
Hata hivyo, Rais Macron amesema kuwa Ufaransa itasitisha hatua za kufikia makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini.