Timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania Bara chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) imetinga hatua ya robo fainali kibabe kwa kuibanjua Zanzibar mabao matano kwa sifuri, katika michuano ya Afrika mashariki na kati (CECAFA-U20) inayoendelea nchini Uganda.
Mshambuliaji hatari wa Ngorongoro Heroes Kelvin John alifunga mabao matatu huku mengine yakifungwa na Lusajo Mwaikenda na Novatus Dominic.
Kelvin alifunga mabao yake katika dakika ya 51, 87 na 90+1, huku Mwaikenda na Dominic wakihitimisha kalamu hiyo ya Ngorongoro Heroes dhidi ya ndugu zao wa Zanzibar.
Katika mchezo huo, timu ya Zanzibar ilikua ikitafuta ushindi ili iweze kufuzu robo fainali baada ya kuwafunga Ethiopia bao 2-1, juzi ikishika nafasi ya tatu kwenye kundi B, huku Ngorongoro wakiwa tayari wamefuzu hatua hiyo baada ya kuwafunga Ethiopia mabao 4-0 kabla ya juzi kutoa sare ya 2-2 dhidi ya Kenya.