Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amewataka binadamu wote kulainisha mioyo na nafsi zao ili kusaidia kutokomeza ukiukwaji wa haki za binadamu.
Akitoa neno wakati wa Misa ya Krismas iliyofanyika nje ya Kanisa la Mtakatifu Peter lililoko Vatican, Rome, Papa Francis amekemea ukuta unaojengeka kuwatenga watu wanaohangaika kutafuta nafuu ya maisha yao kwa njia halali. Pia, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliomba dhidi ya majanga ya asili yanayoikumba dunia katika nchi mbalimbali.
Aidha, Papa Francis aliyekuwa akizungumza mbele ya umati mkubwa wa waumini wa dini hiyo, aliwaombea heri watu wote walioshtakiwa kutokana na kueneza dini katika nchi mbalimbali hususan wamishionari na wengine waliotekwa na makundi mbalimbali ya kigaidi.
“Mwenyezi Mungu alainishe mioyo yetu na kuifanya kuwa mifereji ya upendo. Akalete tabasamu lake kwenye sura zetu zilizokosa furaha, na kwa watoto wote duniani: Na kwa wote waliotengwa na wanaoteseka kutokana na machafuko,” ameomba Papa Francis.
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Kanisa Anglican na na mwangalizi wa zamani wa Kanisa la Scotland, wametoa ujumbe wa pamoja wakiisihi dunia yote kuhakikisha inasambaza upendo na amani badala ya chuki na vita.