Walimu wa shule ya Mijongweni, wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro hawana huduma za vyoo kwa zaidi ya mika 10 hali inayowalazimu kujisaidia kwenye choo cha zahanati moja iliyopo jirani na shule hiyo.

Ofisa mtendaji wa kata ya mnadani, Sembuli Mkilaha amebainisha hayo wakati akipokea msaada wa vifaa vya ujenzi wa choo cha walimu katika shule hiyo ambao utatatua adha hiyo ya muda mrefu.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye amenikuliwa na gazeti la Nipashe amesema kwenye zahanati walimu wanatumia choo chenye shimo moja tu.

“Walimu waliopo katika shule hii wanatumia choo kimoja kilichopo pale na wakati mwingine wanapanga folieni kusubiri huduma hiyo kitu ambacho siyo kizuri” alisema mkazi huyo.

Hadi sasa tayari Halmashauri ya wilaya hiyo kupitia mkurugenzi wake, Yohana Sintoo, imekabidhi mifuko 20 ya saruji kwa ofisa mtendaji wa kata ya mnadani.

Akikabidhi mifuko hiyo, Sintoo amesema saruji hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya katibu tawala wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Hatibu Kazungu ambaye aliahidi kuchangia kwaajili ya kuanza ujenzi wa choo hicho.

Awali akizungumzia ujenzi wa choo hicho, Mkilaha amesema ujenzi unatarajia kukamilika katika kipindi kisichozidi miezi sita na unakisiliwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 16.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Omari Mgalla ametoa shukurani kwa mchango huo na kuahidi utatekelezwa katika ujenzi wa choo kama ilivyokusudiwa.

Video: Magufuli aongeza muda usajili laini za simu
Klopp : kuishinda Leicester ni kazi