Shirikisho la soka nchini TFF limetangaza utaratibu utakaochukuliwa dhidi ya wachezaji wa kigeni, ambao wamerejea nyumbani katika kipindi hiki ambacho ligi zimesimamishwa, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Corona ambao umeingia nchini.
Utaratibu huo umetangazwa rais wa TFF Wallace Karia, kwa kusema wachezaji wote wa kigeni hapa nchini iwapo wataondoka na kurejea kwao, hawataruhusiwa kurudi tena nchini kwa ajili ya tahadhari dhidi ya Corona.
Karia amesema kuwa, ligi kuu ya soka Tanzania bara imesimamishwa na Serikali, ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari kwa ajili ya Virusi vya Corona hivyo wanaondoka na kwenda nje ya nchi huko hawatambui aina ya maambukiza yapo kwa kiasi gani.
“Hawajapewa likizo wachezaji bali ligi imesimama kwa ajili ya tahadhari ambayo inachukuliwa kwa sasa, kwa wachezaji wa kigeni watakaokwenda kwenye nchi zao katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama, hawataruhusiwa kushiriki ligi ikiwa ni sehemu ya tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona.
“Tutawasiliana na mamlaka husika ili kuona namna gani tutawazuia na hawataweza kushiriki kwenye ligi iwapo hali itatulia kwani tahadhari kuchukuliwa ni muda wote na sio muda mfupi,” amesema.
Klabu zote za ligi kuu ya soka Tanzania bara na madaraja ya chini zimetangaza kuvunja kambi na kuwaruhusu wachezaji kurudi nyumbani kwa muda wa siku 30, ili kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona.