Waziri wa afya Nchini Kenya Mutahi Kagwe amethibitisha kuongezeka kwa visa saba vya maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo na kufikia 38
Akizungumza katika kikao na wanahabari siku ya Jumamosi waziri wa afya Kagwe amesema kwamba idadi ya visa vya maambukizi nchini Kenya imeongezeka huku mtu mmoja akiripotiwa kufariki na wengine wakipona maambukizi hayo.
Kagwe amesema kwamba kufikia sasa mji mkuu wa Nairobi unaongoza kwa maambukizi ya visa 28, kati ya visa hivyo saba kuna Wakenya wanne, raia wawili wa DR congo na raia mmoja wa China.
Ameongezea kwamba idadi hiyo ni miongoni mwa watu 81 ambao walifanyiwa vipimo katika maabara tofauti nchini humo katika kipindi cha saa 24.
Aidha waziri huyo ametoa habari njema na kusema kuwa wagonjwa wawili waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona wamepona
”Mgonjwa wetu wa kwanza na watatu wamepona virusi hivyo , watafanyiwa vipimo vingine katika kipindi cha saa 48 , tuna matumaini kwamba vipimo hivyo vya pili vitabaini kwamba wamepona kabisa ili kuruhusiwa kutoka katika vituo vyetu vya tiba”, alisema.
Ameongeza kuwa “Mimi mwenyewe ni mwanangu amewekwa karantini . Pia nina mpwa wangu ambaye amewekwa karantini . Tunachosisitiza ni kwamba wakati mtu anapowekwa katika karantini anajilinda yeye na maisha ya wengine,”