Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) imewaomba wamiliki wa mabasi ya shule yaliyokuwa yanatoa huduma za kuwasafirisha wanafunzi kufanya kazi za kuwasafirisha abiria kama ‘daladala’.
Uamuzi huo umefikiwa ili kusaidia kupunguza uhaba wa huduma ya usafiri wakati ambapo kuna watu wamelazimika kutosimama ndani ya daladala kama sehemu ya hatua za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vipya vya corona (covid-19).
“LATRA inawaomba watu binafsi, shule au taasisi nyingine ambazo zina mabasi kuomba leseni ya muda kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri kwenye majiji,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Mamlaka hiyo.
Imeongeza kuwa waombaji wanapaswa kuwasilisha maombi yao kwenye ofisi yoyote ya LATRA iliyo karibu na eneo lao.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe ameeleza kuwa uamuzi wa kutumia mabasi ya shule zaidi unatokana na uhakika kuwa madereva wanaotumika kuendesha magari hayo huwa na vigezo. Vigezo hivyo ni pamoja na kuwa na umri usiopungua miaka 30.
Alisema kuwa hivi sasa hakuna msongamano wa magari kwakuwa magari mengi yalikuwa yanayotoa huduma kwa wanafunzi, hivyo wameona ni busara yakatumika.