Uongozi wa Young Africans umeshauriwa kuingia katika vita ya kumuwania beki wa kati na nahodha wa Coastal Union Bakari Nondo Mwamunyeto, ambaye amekua gumzo kwa siku za karibuni, kutokana na kiwango chake.
Ushauri huo kwa viongozi wa Young Africans, umetolewa na beki Kelvin Yondani ambaye amehudumu ndani ya klabu hiyo kwa zaidi ya miaka mitano.
Yondani amesema atafurahi kama uongozi wa klabu hiyo wataingia kwenye vita na kufanikisha hatua ya kumsajili Mwamunyeto, ambaye pia anahusishwa na mipango ya kusajiliwa na mabingwa wa nchi Simba SC.
“Itapendeza kumuona Mwamunyetoa anacheza Young Africans msimu ujao, ana kiwango kizuri sana na amekua msaada mkubwa katika kikosi chake cha Coastal union pamoja na upande wa timu ya taifa Taifa Stars,”
“Umahiri wake unadhihirisha wazi anaweza kucheza kwa kujiamini, hata ikitokea beki kama mimi na wengineo hapa Young Africans wanapokosekana uwanjani, mashabiki hawatokua na hofu dhidi yake, kwangu huyu ndio chaguo sahii.”
Hata hivyo Mwamunyeto bado ana mkataba na klabu ya Coastal Union, na endapo klabu yoyote itahitaji saini yake mwishoni mwa msimu huu italazimika kutoa kitita cha pesa, ili kufanikisha usajili wake ambao unadhaniwa huenda ukavuka zaidi ya milioni 50.