Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanatulia nyumbani hawajihusishi na ngono katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kwa muda usiojulikana.
Mwanri ametahadharisha kuwa mtoto yeyote atakayerudi shuleni na mimba atachukuliwa hatua yeye na wazazi wake.
“Shule zitakapofunguliwa kazi ya kwanza tutakayofanya ni kuwapima watoto wa shule zote, yeyote atakayekutwa na ujauzito atachukuliwa hatua yeye, mzazi au mlezi wake” amesema RC Mwanri.
Amemuagiza mganga mkuu wa mkoa, dkt. Honoratha Rutatinisibwa, kwa kushirikiana na waganga wakuu wa wilaya zote kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo na mwanafunzi yeyote atakayekutwa na ujauzito hatua kali zichukuliwe haraka iwezekanavyo.
Mwanri ametoa onyo hilo jana katika mdahalo maalum wa wadau wa maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha afya Tabora.
Awali mratibu wa wajasiliamali wa mkoa huo, Asha Mwazembe aliwataka wazazi na walezi kuwachunga watoto wao kwani baadhi ya wanafunzi wameachwa huru hawasomi wamekuwa wakizurura mitaani badala ya kukaa nyumbani kujisomea.