Aliyewahi kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Young Africans Hans van Pluijm amesema utaratibu mbovu wa usajili ndio sababu inayopelekea klabu hiyo kusajili wachezaji wenye viwango vya kawaida.
Pluijm ambaye aliisaidia Young Africans mataji mawili mfululizo ya ligi kuu misimu ya 2014-15 na 2015-16, amesema ili kupata wachezaji wazuri sokoni, klabu hiyo inapaswa kurudi kwenye utaratibu wa kutumia mawakala wazoefu.
Pluijm aliyewahi kuvinoa vikosi vya klabu za Singida United na Azam FC, amewataka mabosi wake hao wa zamani kuacha kusajili wachezaji kwa kutumia taarifa za mitandaoni, kwani mara nyingi taarifa hizo hasa video zinazowekwa Youtube kuwahusu wachezaji hao ni zile ambazo wameonekana kufanya vizuri.
“Nimeifuatilia Young Africans nimegundua wanakosea kwenye usajili, kwani wanasajili wachezaji kutoka nje wa kiwango cha chini na kushindwa kuonesha ushindani, lakini hawajachelewa, kama wanahitaji wachezaji wazuri wanatakiwa kutumia mawakala wazoefu,” amesea babu huyo.
Pluijm amesema kama Young Africans wanahitaji kuchukua ubingwa unaoshikiliwa na watani wao Simba, wanatakiwa kuacha kusajili wachezaji kimazoea kama miaka iliyopita, kwani mambo yamebadilika na ikiwa wanahitaji mchezaji mzuri lazima wakubali kupita njia sahihi kwa kutumia Mawakala.
“Unajua siku za hivi karibuni kumeibuka mazoea watu kusajili wachezaji kupitia mitandao, lakini wengi wao wamekuwa wakidanganya na mwisho unapata mchezaji anayekuja kukalia benchi badala ya kuwa msaada kwenye timu.”
Pluijm ni mmoja wa makocha ambao wameacha historia nzuri kunako klabu ya Young Africans katika muda ambao aliinoa timu hiyo.
Kocha huyo raia wa Uholanzi ambaye pia ni mwanachama wa klabu ya Young Africsn, alipewa uanachana na aliyekuwa Mwenyekiti kwa wakati huo Yusufu Manji.