Shirikisho la Soka la nchini Kenya (FKF) limesema hakuna matumaini ya kuendelea na ligi kwa hivi karibuni na matokeo yake, Gormahia wametajwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Ligi Kuu ya Kenya ilisitishwa tangu mwezi March kutokana na janga la Covid-19 bila tarehe rasmi ya kurudi. Hadi wakati huo, Gor Mahia walikuwa wakiongoza msimamo kwa alama 54 baada ya kucheza mechi 23.
Siku ya Jumatano, Shirikisho la Soka barani Afrika CAF, liliandika barua kwa Mashirikisho ya soka kufafanua njia itakayo tumika kumaliza msimu.
Rais wa FKF Nick Mwendwa ameweka wazi: “Unawezaje kumaliza mechi 10 au 11 zilizobaki wakati hatutaweza kucheza ndani ya mwezi Mei na Juni,”
“Wachezaji wamekuwa nyumbani na wanapaswa kuanza mazoezi, kwa hivyo unapataje wikendi za kutosha kucheza mechi? Gor Mahia watapewa taji, tutapeleka jina lao kwa CAF ifikapo Ijumaa. Hakuna mjadala juu ya maswala haya.”
Mwenda pia amethibitisha kupanda daraja kwa Nairobi City Stars. “Nairobi City Stars na timu iliyoshika nafasi ya pili [Bidco United], zote zimepanda daraja”
“Tulianza msimu na sheria, na ni sheria tunazotumia kama FKF. Ni wazi asilimia 68 ya mechi zimechezwa.” Kama kawaida, timu iliyowekwa katika nafasi ya tatu kwenye ligi daraja la pili itacheza mechi mbili-mbili ili kuamua ni nani anacheza kwenye KPL msimu ujao. “Tutakuwa na mechi za playoff”.
(Source: Goal)