Kiungo wa klabu ya Young Africans Balama Mapinduzi ametakiwa kuongeza juhudi ili ajiweke katika mazingira mazuri ya kupata nafasi ya kwenda kucheza soka nje ya nchi.

Balama aliyesajiliwa na Young Africans msimu huu akitokea klabu ya Allince FC, amekuwa katika kiwango cha juu jambo lililomuibua kocha wa zamani wa Stand United Athumani Bilali ‘Bilo’ ambaye kwa sasa anainoa Gwambina FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza.

Bilo amemtaja Balama kama mchezaji wake bora kwenye ligi kuu msimu huu, akimtaka aongeze juhudi zaidi kwani anaweza kupata nafasi kwenda kucheza soka nje ya nchi hasa barani Ulaya.

“Balama ni miongoni mwa wachezaji wa ligi kuu wanaojituma sana ndani ya uwanja. Nimekuwa nikimfuatilia katika mechi mbalimbali ambazo amepangwa, ni mchezaji anayetimiza majukumu yake kikamilifu.”

“Ukiniuliza mchezaji bora kwangu kwenye ligi ni yupi, lazima nikwambie ni Balama kwani ni mmoja wa wachezaji bora niliowahi kuwashuhudia. Anajituma, pia ni mchezaji asiyechoka uwanjani,” Alisema Bilo

Bilo ambaye ameiweka Gwambina FC katika nafasi nzuri ya kupanda ligi kuu, amesema Balama amebakisha muda mfupi kabla ya kupata nafasi nje ya nchi kama ataendelea kufanya vizuri.

Bilo ni kocha wa pili kumtabiria Balama mambo makubwa kutokana na mambo anayofanya uwanjani, akitanguliwa na aliyekuwa kocha wa Young Africans Mwinyi Zahera ambaye ndiye aliyemsajili, alimtaja kiungo huyo kama miongoni mwa wachezaji wachache Watanzania ambao wanaweza kwenda kucheza soka barani Ulaya.

Wakati akiwa Young Africans, Zahera alimtumia Balama katika nafasi mbalimbali ikiwemo beki wa kulia kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa dhidi ya Zesco United ambao ulipigwa uwanja wa Taifa.

Zahera alimsifu Balama kuwa ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani jambo ambalo linampa kocha wigo mpana hasa pale timu inapokuwa na mapungufu.

Video: Makonda atoa msaada mabati kwa wajane waliothirika na mafuriko
Waziri Jafo: tusione aibu kujifukiza