Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetoa msaada wa vifaa kinga kwa wanachama wa Chama cha Wasioona Tanzania ili kuwawezesha kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) unaosababishwa na virusi vya corona.

Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa viongozi wa chama hicho ni pamoja na vitakasamikono (sanitizers), barakoa, ndoo za kunawia mikono kwa maji tiririka pamoja na sabuni za maji.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa viongozi wa chama, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema OSHA kama taasisi ya umma yenye jukumu la kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa salama, wameguswa na changamoto kubwa inayolikabili kundi hilo maalum katika kujikinga na ungonjwa wa Corona.

“Sote tunafahamu kwamba dunia na nchi yetu ipo katika mapambano dhidi ya janga la Corona ambapo kila mtu anahimizwa kuchukua tahadhari dhidi ya virusi hatari vya
Corona kwa kutekeleza maelekezo mbali mbali yanayotolewa na wataalam wetu wa afya, hivyo kwakutambua changamoto zinazowakumba wenzetu wasioona tumeona ni vema tukawasaidia baadhi ya vifaa kinga muhimu,” ameeleza Mtendaji Mkuu.

Kiongozi huyo mkuu wa OSHA aliongeza kuwa watu wasioona wanakuwa na wakati mgumu zaidi katika kujikinga na Corona kutokana na hali yao ambapo mara nyingi hulazimika kugusana na watu wengine hata wasiowafahamu husasan wanapohitaji
msaada wa kuvushwa barabara au kuongozwa toka eneo moja kwenda jingine.

Aidha amewaomba wadau wengine kujitokeza na kutoa misaada zaidi kwa makundi ya watu wenye ulemavu ili nao waweze kujikinga na kuendelea kushiriki katika shughulimbali mbali za ujenzi wa Taifa.

Akitoa neno la shukrani mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo muhimu, Mratibu wa Idara ya Maendeleo ya Vijana na Chipukizi ya Chama cha Wasiona Tanzania, Omari Itambu, amewashukuru OSHA kwa masaada huo muhimu kwa wanachama wake.

Joto la Uchaguzi Mkuu: Madiwani 8 wa CUF watimkia CCM
DC Mtatiro avunja ndoa ya wanafunzi wa darasa la saba