Kocha mkuu wa Namungo FC Hitimana Thierry amesema ni mapema mno kuanza kuzungumzia mipango ya usajili wa wachezaji ambao watakiongezea nguvu kikosi chake msimu wa 2020/21.
Kocha Hitimana amesema suala la usajili ataanza kulipa nafasi baada ya kukamilika kwa msimu huu wa ligi, ambao utaendelea mwishoni mwa juma lijalo.
Ligi Kuu Tanzania Bara ilisimama kwa miezi miwili kupisha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Kocha huyo kutoka nchini Rwanda amesema kipindi hiki anafikiria namna ya kukiandaa kikosi chake, ili kifanye vyema katika michezo 10 iliyosalia na kumaliza kwenye nafasi nzuri kwenye msiammo wa Ligi Kuu.
“Kwa sasa kuzungumzia kuhusu usajili ni mapema mno, tumebakisha mechi 10 kumaliza ligi pia tupo kwenye michuano ya FA kwahiyo kila kitu kitajulikana baada ya ligi.
Usajili utategemea wachezaji watakao ondoka maana kwa sasa hatujui nani tutakuwa nae na nani ataondoka. Hata sisi kuwa nafasi ya nne hatuwezi kufurahia maana hatujui, michezo 10 kwenye mpira ni mingi tunaweza kushuka au kupanda juu zaidi kwa hiyo baada ya ligi kila kitu kitajulikana.” Amesema Hitimana Thierry
Namungo FC haijaanza kuhusishwa na taarifa zozote kuhusu usajili wa wachezaji kutoka kwenye klabu nyingine nchini.
Wakati huo huo nahodha na mshambuliaji wa klabu ya Namungo FC Lusajo Reliants amesaini kandarasi ya mwaka mmoja kuendelea kuitumikia klabu hiyo hadi 2020.
Lusajo alikua akihusishwa na mipango ya kuwania na klabu ya Young Africans, ambayo aliwahi kuitumikia bila mafanikio.
Mshambuliaji huyo msimu huu wa 2018/19 alifunga mabao 16 katika ligi daraja La kwanza.