Uongozi wa klabu ya Lille Olympique ya Ufaransa umewataka Arsenal FC kuandaa kitita cha pesa cha kutosha, endapo wanahitaji huduma ya mshambuliaji kutoka nchini Nigeria Victor James Osimhen.

Lille Olympique inayoshiriki ligi daraja la kwanza Ufaransa (Ligue 1) wamesema Arsenal wanapaswa kulipa ada inayokaribia ile waliyomchukulia Nicolas Pepe, Pauni 72 milioni.

Osimhen amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akifunga mabao 18 kwenye Ligue 1 huku jambo hilo likimfanya awe kwenye rada za klabu kadhaa wakiwamo Washika Bunduki wa Kaskazini mwa London.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, amekuwa na msimu mzuri huko Ufaransa ambako alitua mwaka jana akitokea kwenye klabu ya Ubelgiji ya Sporting Charleroi kwa ada ya Pauni milioni 10 kwenda kuziba pengo la Pepe.

Mmiliki wa Lille Olympique, Gerard Lopez amesema: “Kuna ofa kadhaa zililetwa. Tulikataa moja kutoka England na nyingine kutoka Hispania kwenye dirisha la Januari. Kuna ofa nyingi zaidi kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini sitaki kutaka majina ya timu zilizoleta ofa hizo.

“Ila ninachowaambia tu kuna ofa nyingi. Lakini, mimi si mtu wa kuuza wachezaji, mwaka jana hata watu hawakuamini kama tungemuuza Pepe kwa sababu tulikataa ofa nyingi sana.”

Wakati huo huo, The Gunners wanafikiria kumsainisha mkataba mpya beki wao wa kati kutoka Brazil David Luiz aendelee kubaki Emirates Stadium baada ya mkataba wake wa sasa kutarajia kufikia tamati mwishoni mwa mwezi huu.

Mwanafunzi akutwa amekufa kwenye tangi la maji
Hitimana Thierry aweka pembeni usajili