Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amefikishwa mahakamani jana katika mji wa Durban ili kujibu mashItaka ya rushwa, udanganyifu na kujitajirisha kinyume cha sheria, kesi ambayo imekuwa ikiunguruma tangu alipong’atuliwa kutokana na tuhuma za rushwa.
Kesi hii inasikilizwa kwa mara nyingine na inahusu biashara ya zamani ya mauzo ya silaha tangu miaka ya 1990, pia anashutumiwa kupokea rushwa kutoka kwa Thomson CSF – jina la zamani la kampuni ya Thales – katika mpango wa mkataba wa mauzo ya silaha wenye thamani ya takribani Euro Bilioni 4 ulioafikiwa mwaka 1999.
Wakati huo, Jacob Zuma alikuwa Makamu wa Rais wa Afrika Kusini na anatuhumiwa kuwa alipokea jumla ya Euro Milioni 50 kutoka kampuni ya Ufaransa ya Thales, ili aweze kupitishia zabuni kampuni hiyo ya Thales.
Afrika Kusini iliamua kutumia zaidi ya dola bilioni 10 kurejelea upya silaha zake, Silaha ambazo nchi hiyo haikuweza kuzihitaji wakati huo na ambazo hazitumiwi, lakini inaelezwa mahakamani kuwa zaidi ya dola milioni 300 zililipwa kama hongo wakati wa mikataba hiyo.