Kamati kuu ya Shirikisho La Soka Barani Afrika (CAF), imefanya mkutano Jana Jumanne (Juni 30, 2020) kupitia video kujadili mustakabali wa michuano mbalimbali ya Afrika, pamoja na masuala mengine kufuatia janga la COVID-19.
Agenda zilizojadiliwa kwenye mkutano huo zilikua nane, na Kamati kuu ya CAF ilifikia mamuzi yafuatayo.
AFCON 2021 (Michuano Ya Mataifa Ya Afrika 2021): Michuano hii imepangwa kuchezwa nchini Cameroon, na imeamuliwa kusogezwa mbele hadi 2022. Tarehe ya kinyang’anyiro cha mwisho na michezo iliyobaki ya kufuzu katika kipute hicho itatangazwa baadaye.
CHAN 2020 (Michuano Ya Mataifa Bingwa Afrika): Michuano hii ilikua imepangwa kufanyika April mwaka huu, imesogezwa hadi Januari 2021 na itachezwa nchini Cameroon.
Rais wa CAF Ahmad Ahmad amesema Kamati Kuu ya CAF imeridhika na nchi ya Cameroon kwa kujitolea kuandaa fainali mbili tofauti.
Msimu wa 2019/20 Klabu Bingwa Afrika: Michuano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa (Total CAF Champions League) na Kombe la Shirikisho Afrika (Total CAF Confederation Cup) itarejea Septemba kwa muundo wa timu nne za mwisho kucheza.
Michezo ya nusu fainali itachezwa katika mkondo mmoja badala ya miwili (Nyumani na Ugenini).
Total CAF Champions League: Mahala pa kuchezwa michezo ya timu nne za mwisho pataamuliwa
Total CAF Confederation Cup: Morocco itaandaa mechi za timu nne za mwisho
AFCON 2020 Kwa Wanawake: Kutokana na mazingira magumu, awamu ya 2020 ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake imefutwa. Wakati huo huo Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake itazinduliwa 2021. Muundo na maelezo mengine yatatolewa baadaye.
CAF Awards 2020 (Tuzo Za Afrika): Tuzo za CAF 2020 zimefutwa. Washirika wakuu wa hafla hiyo, Pickalbatros Group, wamesisitiza kutimiza makubaliano yao ya kimkataba kuelekea hafla mbili zijazo.