Katika kuhakikisha msimu mpya 2020/21 ambao utaanza rasmi mwezi Septemba, wanafanya vizuri na kufikia malengo ya kuwa mabingwa, Azam FC wametangaza mikakati yao ya usajili wa wachezaji wa Kimataifa.
Klabu ya Azam FC imemaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu wa 2019/20 ambao ulifikia tamati jana kwenye viwanja kumi tofauti.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdularim Amin ‘Popat’ amesema wamepanga kufanya usajili kwa maana ya wachezaji wa Kimataifa wenye kiwango cha juu kurejesha ubora wa timu yao.
Amesema usajili huo wataangalia zaidi safu ya ushambuliaji kwa kuleta mchezaji ambaye atakuwa msaada mkubwa katika kikosi kwa msimu ujao wa ligi hiyo.
“Usajili tumemuachia kocha na ameeleza juu ya kufanya usajili wa wachezaji anaowahitaji, ili kuona timu yetu ina rejesha ubora wake hasa msimu ujao kupambana kufanya vizuri na kutwaa ubingwa,” amesea Popat
Amesema msimu ujao utakuwa tofauti na sasa ambayo imemaliza ligi ikiwa nje ya mipango yao na kujipanga kwa msimu ujao inapambana kutwaa ubingwa pamoja na kucheza Michuano ya Kimataifa.
“Msimu huu haukuwa nzuri kwetu mambo hayakwenda tulivyopanga kwa msimu ujao tutakuwa bora, nina imani kila kitu kitakuwa Sawa,” amesema Popat.
Kuhusu kurejea kwa mshambuliaji wao Kipre Tchetche alisema wako katika mpango huo na mambo yakienda vizuri anaweza kurejea ndani ya kikosi cha timu hiyo.