Watoto wawili wa familia moja nchini Kenya, mmoja mwenye umri wa miaka mitatu na mwingine miaka saba, wamefariki dunia wakiwa wamelala kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuzidiwa na hewa chafu ya ‘carbon monoxide’ iliyotokana na jiko la mkaa.
Mama wa watoto hao, Daisy Achieng amekaririwa na vyombo vya habari nchini humo kuwa yeye na wanaye wanne walienda kulala usiku, Ijumaa, Agosti 7, 2020, lakini walipoamka Jumamosi asubuhi alibaini watoto wake wawili kati ya wanne wamefariki dunia.
Katika mahojiano aliyofanya na Redio Ramogi, Achieng’ ambaye ni mkaazi wa Bondo, alisema kuwa aliwasha jiko la mkaa usiku mzima wakiwa wamelala kwasababu kulikuwa na baridi kali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Polisi Jamii ya eneo la Bondo, Juma Abuko, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa mwanamke huyo alibaini watoto wamefariki alipoamka alfajiri.
Watoto wake wengine wawili, mmoja mwenye umri wa miaka nane na mwingine umri wa miaka 7 hawakuathirika.
Miili ya watoto hao ilipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospiitali ya Bondo ikisubiri uchunguzi zaidi.