Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mhandisi Robert Gabriel amesaini makubaliano ya utekelezaji wa Mpango wa kusaidia Jamii (CSR) kwa mwaka 2020 wenye thamani ya Sh bilioni 9.2.
Mkuu huyo wa mkoa ameelezea namna Serikali inavyothamini ushirikiano mzuri uliopo kati kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na jamii ya Geita.
RC Gabriel amesema utekelezaji wa mpango huo wa CSR utanufaisha jamii ya Geita katika maeneo mbalimbali hususa ni miundombinu, afya, elimu na biashara ndogo na za kati.
Naye mkurugenzi mtendaji wa GGML, Richard Jordinson amesema hatua hiyo inatekeleza malengo ya kampuni hiyo kuendeleza ushirikiano na serikali za mitaa na jamii nzima kwa ujumla katika kutambua na kusimamia miradi muhimu kwa mustakabali endelevu wa mkoa wa Geita.
“Tunafurahi sana kuendeleza ahadi yetu kwa Serikali na jamii wenyeji. Katika mwaka huu wa tatu wa utekelezaji wa mpango huu baada ya mabadiliko ya sheria ya madini, ni matumaini yetu kuwa tunaweza kuendeleza tulipoishia katika miradi iliyopita ili kuongeza tija kwa jamii’’ amesema Mkurugenzi Jordinson