Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mpendae visiwani Zanzibar kupitia Chama ha Mapinduzi (CCM), ambaye alipitishwa tena kugombea nafasi hiyo, Salim Abdullah Turky maarufu Mr. White amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo.
Turky, mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, amefariki usiku wa kuamkia leo Septemba 15, akiwa Hospitali ya Tasakhta Global Zanzibar baada ya kuugua ghafla.
Mwaka 2017 Tundu Lissu aliposhambuliwa kwa risasi, Turky alitafuta ndege iliyompeleka Lissu Nairobi na kuwa mdhamani wa deni la kukodi ndege iliyokuwa inamilikiwa na FlightLink.
Akiwa mkoani Njombe katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, Lissu ambaye ni mgombea urais kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), amemlilia Turky na kutoa pole kwa wafiwa.
“Wengi wanasema kuwa kupona kwangu ilikuwa ni miujiza ya Mungu, wanasema kwa usahihi kabisa. Salim Turky alichangia muujiza huo, leo napenda kutoa salaam za pole kwa ndugu, jamaa na familia yake. Mwenyezi Mungu awatie faraja na nguvu kwa msiba huu,” amesema Lissu.
Turky anayefahamika zaidi kwa jina la Mr. White, alizaliwa Februari 11, 1963, na amekuwa Mbunge wa Jimbo la Mpendae tangu 2010, jimbo ambalo alikuwa akiliwania pia katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 28, mwaka huu.