Kocha wa Mabingwa wa soka Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (ASFC) Simba SC Sven Vandenbroeck amesema ni pigo kwake kumkosa kiungo kutoka nchini Brazil Gerison Fraga, ambaye aliumia wakati wa mchezo wa mzunguuko watatu wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United Mara, uliochezwa Jumapili, Septemba 20 Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
Kocha Sven amemzungumzia kiungo huyo, kuelekea mchezo wa mzunguuko wanne wa Ligi Kuu dhidi ya Gwambina FC ambao utachezwa kesho Jumamosi, Septemba 26 Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema Fraga amekua mchezaji muhimu kwenye kiosi chake, na kukosekana kwake kwenye mchezo wa kesho na michezo kadhaa ijayo, litakuwa pigo kubwa.
Hata hivyo amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa Simba SC kwa kusema, wachezaji wengine waliosalia kikosini wapo katika hali nzuri, na amejiandaa kuziba pengo la Fraga.
“Ni mchezaji muhimu kwenye kikosi kama walivyowachezaji wengine, kuumia kwake ni pigo ingawa wapo wachezaji wanaoweza kucheza nafasi yake kwa ufanisi, bado sijapata taarifa ya mwisho ya madaktari ingawa nasoma kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa atakuwa nje kwa mwezi mmoja, tunasubiri ripoti ya mwisho ya madaktari,” amesema Sven.
Taarifa za awali zinasema Fraga atakuwa nje kwa muda wa majuma matatu, hivyo atakosa michezo inayofuata dhidi ya Gwambina FC, Mbeya City na Tanzania Prisons na watani zao wa jadi Young Africans utakaochezwa Oktoba 18, Uwanja wa Benjamin Mkapa.