Sakata la aliyekuwa Mchezaji wa Young Africans Bernard Morrison ambaye kwa sasa anakipiga katika Klabu ya Simba limechukua sura mpya , baada ya waajiri wake wa zamani kudai kuwa mkataba baina ya pande hizo mbili yaani Morrison na Simba ni batili.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema wamegundua mkataba ambao umewasilishwa ndani ya Shirikisho la soka nchini TFF kuwa ni batili baada ya kutokuwepo kwa saini ya Kiongozi yoyote wa Simba , badala yake ipo ya Mchezaji huyo pekee na Wawakilishi wake.
Mwakalebela pia amesema katika mtandao wa usajili wa Shirikisho la soka Duniani FIFA yaani Transfer Matching System (TMS) Jina la Mchezaji huyo linasomeka kuwa bado ni Mchezaji halali ya Yanga.
Kwa mujibu wa Mwakalebela tayari wamewasilisha malalamiko hayo TFF ,kuwa kama mkataba wao na Mchezaji huyo ulikuwa batili basi na mkataba kati ya Simba na Mchezaji huyo ni batili kwa sababu umesainiwa na upande mmoja.
Kuhusu rufaa waliyoikata kwenye Mahakama ya kimataifa ya usuluhishia wa michezo CAS kuhusu Mchezaji huyo , Mwakalebela anasema tayari wameshajibiwa hatua ya kwanza na wanatarajia kupata tena taarifa ndani ya siku 15 zijazo.