Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini (NEC), imekanusha madai yaliyotolewa na mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kuwa hakupewa taarifa.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, katibu wa kamati ya maadili ya kitaifa ya NEC Emmanuel Kawishe, amesema tume hupeleka taarifa kwa makatibu wakuu wa vyama na wao hufikisha taarifa kwa wagombea.
“Tume haimpelekei taarifa mgombea mmoja mmoja, taarifa inapelekwa kwa makatibu wakuu wa vyama vyao, hivyo madai ya Tundu Lissu kuwa hajapokea taarifa ni uongo,” amesema Emmanuel Kawishe.
Aidha katibu huyo amesisitiza kuwa Lissu anatakiwa kutimiza adhabu aliyopatiwa kwakuwa imetolewa na tume yenye mamlaka na inayotambulika kisheria.
“Adhabu inatakiwa kutekelezwa kwa kuwa imetolewa na chombo chenye mamlaka ya kisheria na kwa kuzingatia utaratibu, mgombea urais wa CHADEMA anatakiwa kuheshimu na kutekeleza adhabu hiyo kama ilivyotolewa,” amesisitiza Kawishe.
Licha ya NEC kumuadhibu Lissu kutofanya kampeni kwa siku 7, mwenyewe alikaririwa na vyombo vya habari jana Oktoba 2, akisema anaendelea kujianda na mkutano wa kampeni wa siku ya Jumapili Oktoba 4 mpaka pale kamati kuu ya chama chake itakaposema vinginevyo.