Rais wa Marekani Donald Trump amepelekwa hospitali akiwa na homa baada ya kuthibitishwa kuwa na virusi vya corona.

Ikulu ya Marekani imesema Trump alikuwa akijihisi mchovu lakini hali yake iko sawa na amepelekwa hospitali ya jeshi la taifa ya Walter Reed kama hatua ya kuchukua tahadhari.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Trump alipata matibabu ya sindano akiwa Ikulu baada ya mke wake Melania Trump kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa Covid-19.

Aidha, Trump amepelekwa hospitali chini ya saa 24 baada ya kuthibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Usiku wa kuamkia jana Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter, alitoa taarifa kuwa vipimo vimebaini yeye na mkewe Melania wana maambukizi ya Covid 19.

Taarifa hizo zinawadia ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi wa urais ambapo atakabiliana na mpinzani wake Joe Biden.

Sudan na waasi kusaini mkataba wa amani
NEC yasisitiza adhabu ya Lissu iko palepale