Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, ametaja sababu za kukata jina la aliyeongoza kura za maoni katika jimbo la Kawe, Furaha Dominic ambaye ni mtoto wa dada yake na kumchagua Mchungaji Gwajima.
Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 9, 2020, katika mkutano wa kampeni wa chama hicho Jiji la Dar es Salaam, wakati akijiombea kura na kuwaombea kura wagombea udiwani na ubunge ndani ya jiji hilo.
“Naomba niwaambie huyu ni Askofu ni mkweli sana, na ndiyo maana nataka niwaeleze ukweli, aliyeongoza kura za maoni Kawe ni mtoto wa dada yangu, nilimkata jina kwa sababu hawezi akashindana na Gwajima, wa Kawe naomba wamlete Gwajima akajime kweli kweli”, amesema Dkt. Magufuli.
Hata hivyo Dkt.Magufuli, ameonyesha kushangazwa na mgombea urais aliyeshangaa upana wa barabara ya Kimara hadi Kibaha.
“Hii barabara ya Kimara, Kibaha nilisikia mgombea wa urais akilaumu kwamba tunajenga barabara pana na kwamba ametembea nchi nyingi hajawahi kuona, majibu yake ni kwamba si kweli kwamba barabara hii ni pana kuliko zote Duniani” amesema Dkt. Magufuli.