Kikosi cha vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC kimewasili jijini Mbeya mapema leo asubuhi kikitokea Dar es salaam, tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa saba wa ligi hiyo dhidi ya Ihefu FC.
Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria (Zaka Zakazi), amesema kikosi cha wachezaji 20 na viongozi kiliondoka Dar es salaam mapema hii leo kwa usafiri wa anga, na kimewasili salama jijini humo.
Amesema dhumuni kubwa wa kikosi chao kuelekea mpambano huo wa kesho ni kuhakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi kama walivyofanya kwenye michezo sita iliyopita, ambapo yote kwa pamoja walifanikwa kukusanya alama 18, ambazo zinawaweka kileleni.
“Tumefika salama jijinji Mbeya, kwa sasa wachezaji wapo hotelini kwa mapumziko, jioni watafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sokoine ili kukamilisha Program ya benchi la ufundi.”
“Dhumuni la kikosi chetu ni kuhakikisha kinapata alama tatu muhimu ambazo zitaendelea kutuweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, tunajua hilo linawezekana, japo tunawaheshimu wapinzani wetu.” Amesema Zaka.
Wachezaji wa Azam FC waliotua jijini Mbeya tayari kwa mchezo dhidi ya Ihefu FC ni Beko, David, Wadada, Abdul, Bruce, Agrey, Mudathir, Djodi, Chirwa, Tigere, Domayo, Sebo, Niyonzima, Nado, Daniel, Akono, Lyanga, Yakubu, Sure na Prince
Azam FC watapambana na Ihefu FC itakayokua na kocha mpya Zubeir Katwila, ambaye alithibitishwa jana Jumapili kuwa mkuu wa benchi la ufundi la klabu hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu, akichukua nafasi ya Maka Mwalwisi aliesitishiwa mkataba wake mwanzoni mwa mwezi huu, kufuatia kuwa na matokeo mabovu.