Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amezindua safari za Treni ya abiria kati ya Dar es Salaam na Arusha zilizokuwa zimesimama kwa takribani miaka 30 iliyopita.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Arusha leo Oktoba 24, Rais Magufuli amesema kufufuliwa kwa Reli hiyo kutapunguza bei ya bidhaa, gharama za usafiri pamoja na kurahishisha usafirishaji wa mazao ya bustani.
“Leo nimefurahi sana kuja hapa Stesheni ya Arusha kuzindua usafiri wa Reli kutoka DSM,Tanga,Korogwe hadi Arusha ambao ulikuwa umesimama kwa miaka 30, miundombinu ya usafiri ni kichocheo kikubwa cha ustawi wa shughuli za kiuchumi ikiwemo Utalii,Biashara na kadhalika” amesema Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amesema baada ya uchaguzi kukamilika Serikali imejipanga kununua vichwa vya treni 39 na mebehewa 800 ya kusafirishia mizigo na 37 ya abiria.
“Ukosefu au ubovu wa miundombinu ya usafiri ni kikwazo kikubwa cha ustawi wa shughuli za kiuchumi, Tafiti zinaonesha ukosefu ama ubovu wa miundombinu ya usafiri unapunguza pato la Nchi za Afrika kwa 2% na kuongeza bei ya bidhaa kwa 40%” -JPM
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwa mfano Afrika kwa mashirika yanayofanya biashara na kufanya kazi kwa kuhudumia wananchi wake ikiwemo wanyonge na kuwataka watanzania kulinda miundombinu ya treni ili iweze kuwasaidia.
“Ujio wa treni hii hapa Arusha, uchumi wake utapanda, watu watafanya biashara, hata mama lishe watapeleka vyakula vyao kwa viongozi wa treni na abiria wanaoteremka, wenye nyumba za kulala wageni watapata wateja kwa mpigo hivyo ujio wa treni hii ni suluhisho kwa ajili ya kujenga uchumi wa maeneo haya,” amesema Magufuli.
Mara baada ya uzinduzi huo Rais Magufuli ambaye pia ni mgombeautais kwa tiketi ya CCM ameendelea na mikutano yake ya kampeni mkoani humo.