Taifa la Senegal limekua la kwanza kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2022, baada ya kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Guinea Bissau jana Jumapili.
Mshambuliaji wa klabu ya Liverpool ya England Sadio Mane, aliifungia Senegal katika dakika ya 84 na kuikatia tiketi nchi yake ambayo mwaka 2019 ilifika hatua ya fainali na kupoteza dhidi ya Algeria.
Ushindi huo wa ugenini katika mchezo huo uliochezwa jijini Bissau, umeifanya Senegal ifikishe alama 12 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu mbili kati ya tatu zilizopo Kundi I.
Kufuzu huko kwa Senegal ni mafanikio makubwa kwa kocha wao Aliou Cisse, ambaye aliwahi kuwa nahodha wa zamani wa timu hiyo kwani ameandika historia ya kuiongoza Senegal kufuzu AFCON mara mbili mfululizo.
Kwa upande mwingine, bao pekee la Mane lililoivusha Senegal, limemfanya mshambuliaji huyo wa Liverpool kuzidi kusakafia rekodi yake ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Simba wa Teranga.
Mane amefikisha jumla ya mabao 20 na anayemfuatia ni mshambuliaji Mamadou Niang, ambaye kwa sasa amestaafu kuitumikia timu hiyo ya Taifa.
Mshike mshike wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Afrika (AFCON) 2022 utaendelea tena leo kwa michezo kadhaa kuchezwa.
6:00 Malawi vs Burkina Faso
16:00 South Sudan vs Uganda
16:00 Sao Tome vs South Africa
19:00 Gambia vs Gabon
19:00 Mozambique vs Cameroon
16:00 Zimbabwe vs Algeria
19:00 Botswana vs Zambia
16:00 Eswatin vs Congo