Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia, amewaomba Watanzania kuiombea Taifa Stars ili iweze kushinda kwenye mchezo wake wa marudiano dhidi ya Tunisia itakayopigwa kesho Jumanne.

Karia ametoa ombi hilo mapema leo wakati akiipokea Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya umri wa miaka 17 (U17), walipotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakitokea Afrika Kusini ambako walishinda ubingwa wa COSAFA.

Amesema endapo watanzania kwa pamoja watashikamana na kuelekeza dua zao kwa mungu, ana uhakika ushindi kwa Taifa Stars utapatikana kwenye mchezo wa kesho ambao watacheza dhidi ya Tunisia

“Tushikamane kwa pamoja, kila mmoja amuombe Mungu ili atuwezeshe kushinda mchezo wa kesho Jumanne, nina imani hakuna linaloshindikana mbele ya Mungu.” Amesema Karia.

Mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo Novemba 13 (Ijumaa) mjini Tunis, Taifa Stars ilikubali kufungwa bao moja kwa sifuri kwa njia ya mkwaju wa Penati.

Kikosi cha Taifa Stars kiliwasili nchini mapema juzi Jumamosi kikitokea mjini Tunis, na tayari kimeanza maandalizi ya kuelekea mchezo huo ambao utachezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam saa nne usiku.

Wakati huo huo shirikisho la soka barani Afrika CAF limetangaza waamuzi watakaochezesha mchezo huo.

Mwamuzi Celso Armindo Alvacado, raia wa Msumbiji ndio ‘Pilato’ atakayepuliza kipyenga kesho Jumanne, akisaidiwa na Arsenio Chadreque Marengula (Msumbiji), Zacarias Horacio Baloi (Msumbiji), Simoes Bernardo Guambe (Msumbiji), mwamuzi wa akiba, Dlamini Zide Gilbert (Eswatini), Kamishna wa mchezo na Mfubusa Bernard (Burundi) ndio mtathmini waamuzi.

Ronaldo akaribia UNITED, Juventus wamgwaya
Simba wa Teranga atangulia AFCON 2022

Comments

comments