Waziri wa Maji Juma Aweso, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Antony Sanga, kuhakikisha Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dodoma (DUWASA), inachimba visima viwili vya maji vyenye uwezo wa kuzalisha ujazo wa mita za maji 400 kila kimoja kwa saa, sawa na lita 400,000 ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya maji kwa wakazi wa Dodoma.
Idadi hiyo itafanya Dodoma iwe na visima vitatu vikubwa vyenye uwezo wa kuzalisha ujazo wa mita za maji 1,200 sawa na lita milion 1.2 kwa saa, maji ambayo yatakidhi mahitaji ya wananchi wa Dodoma.
Akizungumza katika ziara ya kushtukiza ya kutembelea ujenzi wa kisima cha maji unaoendelea katika eneo la Mzakwe, Waziri Aweso amesema visima hivyo vikiongezwa vitasaidia kuziba pengo linalopelekea maeneo mengine kukosa maji.
Sambamba na hilo, Aweso amesema Tanzania ina rasilimali nyingi za kutosha, hivyo wao kama wizara ya maji watatumia vyanzo vya maji vya ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Mto Rufiji na Mto Ruvuma kusambaza maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph, amesema kisima hicho kina ukubwa wa mita 150 na mpaka sasa wamefikia hatua ya moja ya tatu ya kukamliisha ujenzi wa kisima hicho.