Uongozi wa Klabu ya Ruvu Shooting unaamini endapo kikosi chao kingepata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021, kingetinga hatua ya fainali na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu huko Mlandizi mkoani Pwani, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino Masau Bwire amesema kikosi chao msimu huu kipo imara na kulingana na kasi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, wameona walikua wanatosha kwenda Zanzibar kushiriki na kufanya maajabu.
Amesema mwaka huu timu zilizoshiriki michuano hiyo ambayo hutumika kama sehemu ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, zimeonyesha kiwango cha kawaida ukilinganisha na uwezo wa kikosi cha Ruvu Shooting ambacho kwa upande wa Ligi Kuu msimu huu 2020/21 kimekua tishio kubwa.
“Hatukupata fursa hiyo, ipo siku tutaipata, na hali ikiwa kama ilivyokua msimu huu na timu zikacheza kama zilivyocheza, hakuna timu ambayo itaweza kutuzuia kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.”
“Mimi nina hakika katika hilo, uwezo wetu kwa sasa ni mkubwa sana na tunazidi kukiimarisha kikosi, ili tutakapokua kwenye mashindano kama hayo, tuweze kuacha historia kubwa kwa vizazi vijavyo.” Amesema Masau.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021 ilifikia tamati jana usiku kisiwani Unguja-Zanzibar, kwa kikosi cha Young kuibuka mabingwa kwa kuwabanjua Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kwa changamoto ya mikwaju ya penati nne kwa tatu.
Timu zilizoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu 2021 kutoka Zanzibar ni Jamhuri, Chipukizi, Malindi FC na Mlandege, huku Young Africans, Simba SC, Namungo FC na Azam FC zikitokea Tanzania Bara.