Baraza la Seneti nchini Marekani limepiga kura kuendelea na mchakato wa mashtaka dhidi ya rais wa zamani Donald Trump, likisema mchakato huo ni wa kikatiba.
Baraza la Seneti lilipiga kura 56 kwa 44 za kuendelea na kesi dhidi ya Trump, likizipinga hoja za mawakili wake kwamba rais hawezi kushitakiwa pindi anapomaliza muda wake.
Maseneta ambao waliapishwa kama wazee wa baraza, walipitia picha za vidio za wafuasi wa Trump wakipambana na polisi, kuvamia kumbi za bunge na kupeperusha bendera za Trump ambapo kuliwasilishwa vidio za Trump mwenyewe akiwahimiza wafuasi wake kabla ya uvamizi kuwa wapambane hadi tone la mwisho kupinga kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa Novemba 3.
Aidha, Mawakili wa Trump wameendelea kuushambulia mchakato huo wakisema ni kinyume na katiba na kwamba ni juhudi za kumzuia kiongozi huyo kuwania tena nafasi ya urais.
Hata hivyo, Wakili anayeongoza jopo la utetezi upande wa Trump Bruce Castor, amesema mashitaka dhidi ya rais huyo hayahitajiki tena kutokana na kwamba kiongozi huyo aliondolewa madarakani kupitia kura na hivyo lengo la kikatiba tayari limefanikiwa.
Ikumbukwe Trump ni rais pekee kushitakiwa katika baraza la seneti baada ya kumaliza muda wake madarakani na wa kwanza kushitakiwa mara mbili. Mchakato huo unaendelea leo chini ya ulinzi mkali katika maeneo yote ya bunge.