Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF” limefanya uteuzi wa maafisa Afya watakaendesha zoezi la upimaji wa COVID-19 kwa michezo ya Ligi ya Mabingwa ya CAF na Kombe la Shirikisho itakayochezwa mwishoni mwa juma hili.
CAF wamefanya uteuzi huo ili kuepuka figisu figisu ambazo huenda zikafanywa na timu mwenyeji, kufuatia utaratibu wa awali kutoa nafasi kwa nchi mwenyeji kupima na kutoa majibu ya vipimo vya Corona.
Hata hivyo uteuzi huo wa maafisa wa Afya utakaofanywa na CAF, hautowahusisha maafisa wa ndani ya nchi mwenyeji wa mchezo jambo ambalo hapo awali lilikuwa liliwahusisha maafisa wa ndani ya nchi hizo.
Huenda CAF wamefanya hivyo kufuatia malalamiko ya badhi ya klabu za soka Barani Afrika, ambazo hazikuridhishwa na matokeo ya vipimo vilivyofanywa kwenye michezo yao ya mwisho, kabla ya kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na kuchezwa kwa michezo ya hatua ya mtoano kombe la Shirikisho.