Wakili wa ngazi ya juu wa Uingereza Karim Khan amechaguliwa kuwa Mwendesha Mashitaka Mkuu ajaye wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Karim Khan, mwenye umri wa miaka 50, kwa sasa anaongoza uchunguzi wa Umoja wa Mataifa juu ya uhalifu wa kivita unaodaiwa kutekelezwa na kikundi cha Dola ya Kiisalmu (Islamic State) nchini Iraq.
Khan amepata ushindi wa kura 72 kati ya 123 za nchi wanachama katika awamu ya pili ya uchaguzi, na ataanza muhula wake wa miaka tisa katika mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini Hague mwezi Juni mwaka huu.
Amewashinda wagombea wengine kutoka Ireland, Italia na Uhispania, na atachukua mikoba ya Fatou Bensouda, raia wa Gambia.
Amewahi kuwa mtetezi wa Naibu Rais wa Kenya William Ruto katika mahakama ya ICC ambayo ilitupa nje mashitaka ya mauaji, kusafirisha na mateso kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007 na pia mtetezi wa mtoto wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, Saifd Al Islam.
ICC ndio taasisi pekee ya kudumu inayochunguza uhalifu dhidi ya binadamu.