Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amemteua Mkuu wa Shirika la Madini, Jean-Michel Sama Lukonde Kyenge, kuwa Waziri Mkuu mpya, kufuatia mapambano ya muda mrefu ya kuwania madaraka na washirika wa mtangulizi wake Joseph Kabila.
Sama Lukonde, mwenye umri wa miaka 43, anachukua nafasi ya Sylvestre Ilunga Ilukamba, aliyelazimishwa kujiuzulu baada ya muungano kati ya wafuasi wa Tshisekedi na Rais wa zamani Kabila kuvunjika.
Akizungumza baada ya kuteuliwa, Lukonde amewaambia waandishi habari kwamba kurejesha hali ya usalama ndiyo kitakuwa mmoja ya vipaumbele vyake vya juu, hasa katika eneo la mashariki na Katanga, eneo la uchimbaji madini anakotokea.
“Usalama, kama munavyojua, ni moja ya vipaumbele, haswa mashariki mwa Kongo na huko Katanga. Pamoja na maswala ya usalama, tuna pia maswala ya kijamii, ile ya maendeleo, maswala ya kisheria na pia swala la elimu kwa wote. Tuligusia mengi kuhusu mageuzi kwani yanahitajika katika sekta kadhaa,” amesema Lukonde.